TAFUTA CHOCHOTE NDANI YA NKEMA

Wednesday, 9 October 2013

ZIJUE FAIDA ZA KULA NDIZI MBIVU

 

Ndizi ni matunda yanayopatikana kila mahali. Siku hizi kila penye kioski au grocery ya matunda ni rahisi kupata ndizi. Ndizi hizo huuzwa kwa bei ya kawaida tu kwako kuweza kununua. Ndizi ni tunda lenye rangi ya kijani liwapo bichi na rangi ya njano likiwa limeiva vizuri. Tumezoea kuona ndizi kwenye migomba shambani au vichane vya ndizi sokoni tunapokwenda kununua vitu mbalimbali kwaajili ya mlo. Swali ni, je tumeshawahi kujuiliza ni faida gani tunapata tunapokula ndizi hizo?


Labda huu ni wakati sahihi sasa tujue manufaa ya kula ndizi mbivu. Na hapa ni baadhi ya faida za kula tunda hili zuri na lenye lanya tamu.

1. Ndizi ni tunda lenye vitamin nyingi na madini kadhaa.
-Vitamin B6 na C hupatikana kwenye ndizi. Vitamin B6 ipo katika kiwango kikubwa kwenye ndizi ukilinganisha na Vitamin C ambayo ni kidogo. Madini yanayopatikana kwenye ndizi ni magnesium, manganese na potassium. Madini ya magnesium na manganese yana compound inayojulikana kama ‘’cytokinin’’ ambayo huongeza idadi ya chembe chembe nyeupe za damu hivyo huboresha na kuongeza kinga ya mwili. Madini ya potassium nayo husaidia kudhibiti shinikizo kubwa la damu (high blood pressure) na kuimarisha utendaji kazi wa moyo. Vile vile madini ya potassium huzuia upotevu wa madini muhimu ya calcium mwilini ambayo hutumika katika utengenezaji wa mifupa. Kwa kifupi vitamins na madini yanayopatikana kwenye ndizi husaidia kupambana na seli za saratani.

2. Ndizi husaidia kupambana na vidonda vya tumbo.
-Sio tu kwamba ndizi hupambana na seli za saratani lakini pia hukinga tumbo kupata vidonda vya tumbo kwa uwezo wa compounds mbalimbali  ilizonazo. Compounds hizi zinazopatikana kwenye ndizi hujenga tabaka nene kwenye kuta za tumbo ambazo hukinga tumbo kuathirika na tindikali ijulikanayo kama ‘’hydrochloric acid’’. Pia ndizi zina enzyme inayojulikana kama ‘’protease inhibitor’’ ambayo huzuia bakteria wasababishao vidonda vya tumbo. Huh,…ni faida ilioje. Yani ukila ndizi tu unaweza usimwone daktari kwaajili ya tatizo la vidonda vya tumbo.

3. Ndizi huboresha ngozi.
-Kama ilivyo ngozi yako maganda ya ndizi nayo ni muhimu pia kwani yanaweza kupendezesha kabisa ngozi yako kama yakisagwa vizuri na matunda mengine kama parachichi. Virutubisho hivyo kwa pamoja hulainisha ngozi na kuifanya yenye muonekano mzuri wa kung’aa.

4. Ndizi huongeza nguvu mwilini.
-Ili uweze kufanya kazi zako kwa umahiri ni lazima mwili uwe na nguvu. Ndizi mbivu huwa na sukari ujulikanayo kama ‘’glucose’’ ambayo huongeza nguvu mwilini. Sukari hii inahitajika katika kiasi maalum mwilini.

5. Kambakamba za kwenye ndizi  husaidia kuimarisha mfumo wa chakula.
-Ni kweli kabisa kambakamba za kwenye ndizi husaidia chakula kuteleza vizuri kwenye njia ya chakula. Kwa maana hiyo chakula kinaweza kupita kirahisi bila kipingamizi.

6. Hii labda ndio ulikuwa hujui kabisa ‘’ndizi husaidia kupunguza stress na kukufanya uwe katika mood nzuri.’’
-Unaweza kujiuliza kivipi? Kama ulikuwa hujui ndizi zina kemikali mahsusi iitwayo ‘’tryptophan’’ ambayo iwapo mwilini hubadilishwa na kuwa ‘’serotonin’’. Kemikali hii ya serotonin iwapo mwilini husaidia mtu ajisikie vizuri na kuwa katika mood nzuri na hatimaye kupunguza stress. (msongo wa mawazo)
 
 
 
 By  Kamotta

No comments:

Post a Comment