TAFUTA CHOCHOTE NDANI YA NKEMA

Tuesday, 28 October 2014

Ushauri kwa wanaoanza Elimu ya Juu mwaka 2014

Mwezi huu wa octoba wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na elimu ya juu hapa Tanzania wameanza kuripoti kwenye vyuo walivyopangiwa. Awali ya yote nichukue nafasi hii kuwapongeza wale wote ambao wamepata nafasi ya kuendelea na elimu hii ya juu. Iwe ni kwa nafasi ya cheti, stashahada au hata shahada kuna kazi kubwa umeifanya huko nyuma na sasa unaingia kwenye ngazi nyingine ya elimu.

Leo naomba nichukue muda wako kidogo kukupa ushauri ambao unaweza kuwa msaada mkubwa sana kwako kama utaufuata. Ushauri nitakaokupa hapa sio namna gani ya kusoma maana naamini kwa miaka zaidi ya kumi uliyokaa kwenye mfumo wa elimu, unajua ni jinsi gani ukisoma utafaulu na jinsi gani ukisoma utafeli. Hivyo endeleza mbinu zilizokusaidia nyuma na ziboreshe zaidi ili uweze kupata ufaulu mzuri.

Ushauri mkubwa nitakaokupa hapa ni kuhusu mafanikio na uchumi.

Mpaka sasa umeshaimbiwa sana wimbo huu kwamba nenda shule, soma kwa bidii, pata ufaulu mzuri, utapata kazi nzuri na kuwa na maisha mazuri. Kauli hii ilikuwa kweli zamani ila kwa sasa ina ukweli nusu na uongo nusu. Ni kweli kusoma kwa bidii kutakupatia ufaulu mzuri. Sio kweli kwamba ufaulu mzuri utakupatia kazi nzuri na hivyo kuwa na maisha mazuri. Kama huamini hili utalishuhudia miaka michache ijayo baada ya kumaliza elimu yako.

Ukweli ni kwamba kuna watu wengi wamesoma ila kazi hawajapata na pia kuna watu wengi wana kazi ila bado maisha yao ni magumu sana. Yaani kazi zao zimekuwa kama mtego ambao umewanasa na hivyo hawawezi kuchomoka. Lengo la makala hii ni wewe kujiandaa ili kutokuingia kwenye matatizo haya ambayo yatafanya maisha yako yawe magumu sana.

Kwa kifupi sana naomba nikushauri mambo haya matano na yafanyie kazi sasa ili kuweka maisha yako vizuri.

1. Weka malengo ya maisha yako.

Ni muhimu sana wewe kuweka malengo na mipango ya maisha yako. Malengo haya weka ya muda mfupi na hata ya muda mrefu. Andika ni jinsi gani maisha yako unataka yawe na ni kazi au biashara gani utafanya. Andika malengo yako ya miaka mitano, kumi, ishirini na hata miaka thelathini ijayo. Tumia malengo haya kama ramani yako ya kukufikiasha kwenye maisha unayoyatazamia. Kwa maelezo zaidi kuhusu malengo bonyeza maandishi haya kusoma makala za malengo.

2. Jifunze vitu vya ziada.

Japokuwa umeingia chuoni kusomea ualimu, udaktari, sheria au uinjinia bado unayo haja ya kujifunza mambo mengine ya ziada. Tumia muda wako wa ziada kujifunza mambo mengine ambayo hufundishwi kwenye masomo unayosoma. Kimoja kikubwa cha kujifunza ni kuhusu fedha, ijue sayansi ya kupata na kutumia fedha. Jifunze pia kuhusu biashara na hata uwekezaji. Pia jifunze kwa kujisomea vitabu ambavyo vitakupa mtazamo wa tofauti kuhusu maisha na mafanikio kwa ujumla. Kama huna kitabu cha kuanzia kusoma nitumie email kwenye amakirita@gmail.com nitakutumia vitabu.

3. Endeleza vipaji vyako.

Kila mmoja wetu ana vipaji au vitu ambavyo anapendelea kufanya. Na mara nyingi sana vipaji hivi ni tofauti kabisa na vitu unavyosomea. Tumia muda huu ulipo chuoni kuendeleza vipaji vyako. Fanya mazoezi zaidi ya kile unachopenda kufanya na pia jifunze ni jinsi gani unaweza kutumia vipaji vyako na ukapata fedha. Kama mpaka sasa hujajua vipaji vyako soma; Jinsi ya kugundua vipaji vilivyoko ndani yako.

4. Tengeneza mtandao.

Moja ya faida za wewe kuwepo chuoni sio tu kupata masomo bali pia kujuana na watu mbalimbali. Watu hawa unaojuana nao wanaweza kuwa watu muhimu sana kwako siku za baadae. Hivyo unapokuwa chuoni jenga mtandao wako wa marafiki na hata watu wengine. Mnaweza kukutana watu ambao mna ndoto sawa na baada ya masomo mkaingia kwenye biashara kwa pamoja. Watu wengi wanaoshirikiana kwenye biashara na waliopata mafanikio makubwa walikutana vyuoni.

5. Anza kuweka akiba.

Hapa unaweza usinielewe, ngoja nijitahidi kukuambia taratibu. Iko hivi, kuna tatizo kubwa la ajira, ila kuna fursa kubwa sana kwenye ujasiriamali na biashara. Wenzako wanalalamika kwamba hawana mtaji wa kuanzia biashara au ujasiriamali. Na kwa bahati mbaya hakuna wa kuwapa mtaji huo. Sasa wewe usifuate njia hii, anza sasa kujiwekea akiba ili utakapomaliza masomo uwe na mahali pa kuanzia.

Kama unasoma kwa mkopo wa serikali, hii ina maana unapewa fedha za kujikimu ambazo kwa sasa ni tsh 7500/= kwa siku. Nakushauri hapa ishi maisha ya kawaida sana na kila siku weka akiba tsh 1000/=. Ukifanya hivi. kwa semista moja yenye siku 120 utakuwa umeweka tsh 120,000/= kwa mwaka mmoja wa masomo tsh 240,000. Ukichangia kidogo kutoka kwenye fedha ya mafunzo kwa vitendo unaweza kuweka akiba ya tsh 300,000/= katika mwaka mmoja wa masomo. Kwa miaka mitatu ya masomo utakuwa umeweka karibu milioni moja. Kwa milioni moja, kama umekutana na wenzako wawili ambao mnaendana na mna ndoto sawa na kila mmoja akawa na milioni moja tayari mna milioni tatu, hii sio sawa na bure, mnaweza kuitumia kufanya mambo makubwa sana. Kama ukiweza kuiweka fedha hii kwenye uwekezaji ambao unakupatia asilimia kumi kwa mwaka, kwa miaka hiyo mitatu utapata kiasi kikubwa kidogo. Hii inawezekana kama hutaishi maisha ya kuiga, kwamba mwenzako kanunua ‘sabufa’ na wewe ukanunue ‘sabufa’.

Yafanyie mambo hayo matano kazi na wakati huo ukijijengea tabia ya nidhamu binafsi na kujiamini ili uweze kufikia malengo yako.

Ili kuendelea kupata mafunzo mazuri ambayo yataendelea kukupa hamasa ya kufikia mafanikio makubwa, jiunge na KISIMA CHA MAARIFA. Kupata maelezo zaidi kuhusuKUJIUNGA NA KISIMA CHA MAARIFA bonyeza hayo maandishi.

Nakutakia kila la kheri katika masomo yako.

TUKO PAMOJA.

No comments:

Post a Comment