TAFUTA CHOCHOTE NDANI YA NKEMA

Wednesday, 27 May 2015

BORA KUWA MJINGA KULIKO MZEMBE

Test-your-stupidity-2014
Ujinga na uzembe ni vitu ambavyo vina madhara makubwa sana katika jamii na hasa vikimkuta mtu ambaye anategemewa katika shughuli fulani. Lakini hebu tuangalie maana na tofauti ya vitu hivi viwili kwa ufupi.
Ujinga: hii ni hali ya mtu kutofahamu au kujua kitu fulani, hii hutofautiana sana baina ya mtu na mtu, kwa ujumla unaweza kusema kuwa kila mtu ni mjinga katika jambo fulani ambalo halijui, ni kweli. Unaweza kuwa unajua jambo hili na ukawa hujui jambo lingine, hivyo basi, wewe utakuwa ni mjinga wa jambo lingine usilojua. Lakini huu si ujinga ambao tunauzungumzia hapa.
 
Ujinga tunaozungumzia hapa ni ile hali ya mtu kutofahamu au kujua mambo ya muhimu na msingi katika maisha yake, na hii huwakuta sana watu ambao kwa njia moja au nyingine hawakupata bahati ya kwenda shule.
Uzembe ni ile hali ya mtu kutokuwa makini na jambo au kazi anayofanya hata kusababisha matokeo hasi katika jambo au kazi hiyo. Hii haijalishi uwe umeenda shule au hujaenda, hali hii huweza kuwakuta watu wa aina zote.
Tumekuwa mara nyingi tukipiga sana vita Ujinga. Lakini vita dhidi ya uzembe bado hatujahusika nayo au kama tayari basi ni mara chache sana. Mjinga akielimishwa basi hapo ujinga unapotea kabisa kwani ile sifa ya kutojua jambo inakua imefutika kabisa, na ni rahisi sana kutibu ugonjwa huu wa ujinga kwani kazi yake ni kumuelimisha asiyejua.
Sasa hebu tuangalie uzembe. Unaweza kuwa msomi mkubwa sana lakini ukawa na tatizo hili. Uzembe una madhara makubwa sana kwani huwa ndani ya asili ya mtu tangu enzi na enzi. Ikiwa una tabia hii, basi ni kazi kubwa sana endapo mtu hatofahamu kama yeye ni mzembe.
Si kwamba mtu anazaliwa na uzembe, ila uzembe hutokea baada ya mtu kuwa na tabia fulani ambayo mpaka sasa watu wengi sana tabia hii wanayo.
Hali ya kutojali. Yaani unaweza kuwa mtu wa kutojali jambo lolote lile, hujali mali za watu pale unapomilikishwa, hujali afya yako, hujali mahala unapolala, hujali mazingira yaliyokuzunguka, hujali kama kufanya jambo fulani kutakuletea madhara fulani. Ukiwa na tabia hizi basi hali ya uzembe ni rahisi sana kukupata na utapata athari sana, hasahasa pale utakapokabidhiwa ofisi ya mtu au unatakapoajiriwa.
Ikiwa umeshindwa kujali mazingira unayolala, basi hata ukipewa ofisi ya mtu kufanya kazi hutapajali hata kidogo. Ikiwa umeshindwa kujali mali za watu pale ulipoazimwa au kukabidhiwa, hutajali mali za ofisi ya watu pale utakapo ajiriwa. Na madhara yake ni makubwa sana. Na jambo hili linajulikana sana hata katika mashule tunayosoma, utaona katika ripoti ya mwanafunzi kuna kipengele cha utunzaji wa mali za shule.
Uzembe hukua na kukomaa hasa pale mtu anapokosa dhana ya uwajibikaji. Ukiulizwa wajibu wako lazima utasema wajibu wangu ni huu na huu na huu, lakini ukiulizwa je unatimiza wajibu wako? Hapo jibu linakosekana au kupatikana nusu.
Ili kuepukana na uzembe, jitahidi kufanya mazoezi ya uwajibikaji kwanza, kisha hakikisha unajali kila hali unayokutana nayo na ni vema uige mifano ya mtu fulani ambaye unajua anawajibika na kujali mali, mazingira na hali zinazomzunguka. Usione aibu kutaka ushauri wa kuepukana na hali hii. Kila mzembe anajua kabisa kwamba yeye ni mzembe ila kukubali waziwazi ndiyo inakuwa vigumu sana.
Nakushauri sana kuanzia sasa ikiwa unahisi una hali hii au rafiki au ndugu yako basi anza kumshauri kwa kumpa mifano na madhara mbalimbali ya uzembe.
Uzembe husababisha wagonjwa kufa mahospitalini, husababisha magari kupata ajali, husababisha watu kuibiwa madukani, husababisha vifo vya bahati mbaya, husababisha watu kupata maradhi mbalimbali, husababisha watu kufukuzwa kazi, husababisha wanafunzi kufeli mitihani, husababisha mali kupotea bila kujua, husababisha kuona maisha magumu na kukosa hela, husababisha njaa, husababisha ugomvi baina ya watu, husababisha kukosa upendo kutoka kwa ndugu na marafiki, husababisha kukosa uaminifu. Na mengine mengiiii
Kumbuka uzembe ni adui wako mkubwa sana. Epukana naye utaona faida katika maisha yako, watu watakupenda na kukuamini ukiwa siyo mzembe.Yaani kama unaweza badilika sasa

No comments:

Post a Comment