TAFUTA CHOCHOTE NDANI YA NKEMA

Saturday 9 November 2013

Namna ya Kuondoa kadhia ya ladha chungu mdomoni wakati wa ujauzito

Picture 

Mojawapo ya mabadiliko wanayoyapata baadhi ya wanawake wajawazito ni pamoja na ladha chungu inayokerehesha mdomoni hasa miezi mitatu ya mwanzo ya ujauzito, kitaalamu, huitwa dysgeusia.

Hali hii si jambo la kumshitua mjamzito na kudhani ni dalili kuwa kuna hatari inayojitokeza kwake ama kwa k/viumbe tumboni mwake, bali ni hali inayosababishwa na mabadiliko ya vichocheo (hormones) mwilini hasa kiwango cha estrogen. Vile vile
huweza kuchangiwa na vidonge vya kuongeza vitamini ama vichocheo kadiri alivyokuagiza daktari ama mhudumu wa afya kutumia.

Estrogen huathiri kubadili milango ya hisia zinazohusika na ladha (taste) na kwa kuwa sehemu hii inakaribiana na milango ya hisia za kunusa, wakati mwingine huathiri pia harufu anayovuta mjamzito.

Kwa baadhi ya wajawazito, hali hii si ya kudumu kwa miezi yote ya kipindi cha ujauzito, kwani wengi wameripoti kuwa hundoka baada ya miezi mitatu ya mwanzo ya ujauzito (first trimester) baada ya vichocheo kutulizana mwilini, ingawaje wapo ambao wamesema ilibidi kuishi katika maudhi hayo kwa kipindi kizima cha ujauzito hadi siku chache baada ya kujifungua.

Jinsi ya kupambana na hali hii

Tumia vyakula au vinywaji vyenye asidi ambavyo licha ya kukata ladha chungu mdomoni, pia vitaongeza kiwango cha mate mdomoni ambayo yanasaidia kuosha na kuondosha uchungu wenyewe. Vyakula hivi pia husaidia kurekebisha kiwango cha pH kinachohusika na usahihi wa asidi na alkali mwilini.

  1. Matunda au juisi zenye uchachu/ugwadu kama vile malimao, machungwa, machenza, nyanya, matofaa, ukwaju, mabungo, ng’ong’o, ubuyu, maembe n.k. (hapa ndipo ilipo rahisi kuelewa ni kwa nini wajawazito huonekana wanapenda vitu vichachu)

  2. Weka siki (vinegar) kidogo  kwenye chakula

  3. Tumia chachandu na ‘pickle’ 

  4. Safisha ulimi kwa mswaki mara kwa mara

  5. Sukutua kwa maji yenye chumvi (kwa kipimo cha kijiko kimoja cha chai kwenye bilauri moja ya maji. Unaweza kuongeza ama kupunguza kadiri ulimi wako unavyoweza kuvumilia). 

  6. Sukutua kwa maji yenye magadi/baking soda (siyo baking powder, hivi ni vitu viwili tofauti) kwa kipimo cha robo kijiko cha chai kwa bilauri moja ya maj. Unaweza kuongeza ama kupunguza kadiri ulimi wako unavyoweza kuvumilia)

  7. Tafuna gum (Bazooka, BiG n.k.)

  8. Nunua pipi zenye ladha ya machungwa, malimao au mint

  9. Kunywa maji ama supu au chai ili kusaidia kusafisha ziada ya vichoche inayotolewa mwilini kama sumu. Kwa kufanya hivyo, unaharakisha kuiondoa mwilini na hivyo kupunguza maudhi yake(kama ianvyoshauriwa kunywa maji mengi ukiwa unatumia antibiotic)

  10. Pata ushauri kutoka kwa mtaalamu wa uzazi na wajawazito endapo unatumia vidonge vya vitamin au vichocheo ambavyo vinaweza kuchangia hali hii, yeye atakushauri vyema cha kufanya.

No comments:

Post a Comment