TAFUTA CHOCHOTE NDANI YA NKEMA

Sunday, 3 November 2013

Mwakyusa, Dk Mvungi wavamiwa na majambazi kwa nyakati tofauti

Picha zilizopachikwa hapo juu (bofya moja moja ili kuzikuza) zinatoka kwenye blogu ya Francis Dande "Habari Mseto" zikiambatana na habari ifuatayo kutoka kwa Hapiness Katabazi:

MJUMBE wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba nchini na mhadhiri mwandamzi wa Sheria wa Chuo Kikuu cha Bagamayo (UB), Dk. Sengondo Adrian Mvungi, saa saba usiku wa kuamkia leo amevamiwa na watu wasiyojulikana nyumbani kwake Kibamba nje
 kidogo ya jiji la Dar es Salaam na kumcharanga mapanga maeneo ya mwilini mwake ikiwemo sehemu za kichwani kwa madai kuwa watu hao wanaosadikiwa kuwa ni majambazi walikuwa wakimshinikiza awapatie fedha na Dk Mvungi alipowaambia hana fedha ndipo walipoanza kumcharanga mapanga.

Mtoto mkubwa wa Dk Mvungi, aitwaye Dk Natujwa Mvungi ambaye ni Mkuu wa Shule ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Bagamoyo Dar es Salaam, saa nane usiku alimthibitishia mwandishi wa habari hizi kuwa ni kweli baba yakealivamiwa na kujeruhiwa na mapanga na watu wasiyojulikana.

Dk Natujwa anasema baada ya watu hao kumjeruhi baba yake na kufanikiwa kutoroka, wao walimchukua na kumkimbiza katika Hospitali ya Tumbi mkoani Pwani, na kupatiwa matibabu ya huduma ya kwanza na kisha kumkimbiza katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambapo alisema kwanza alipokelewa katika eneo la dharura na kisha saa kumi na moja asubuhi aliingizwa kwenye wodi ya Taasisi ya Mifupa MOI) kwa ajili ya matibabu.

------

Kisha gazeti la HabariLeo limechapisha taarifa ifuatayo: 


Mhadhiri wa Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es Salaam (CBE), Emmanuel Mwakyusa amefanikiwa kuwasambaratisha majambazi saba aliopambana nao nyumbani.

Majambazi hao walimvamia nyumbani kwake eneo la Pugu jijini Dar es Salaam, ambapo  alifanikiwa kumuua mmoja, kati ya wawili aliowajeruhi. Tukio hilo lilitokea jana saa 8:30 usiku.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.

Alisema Mwakyusa aliwajeruhi majambazi wawili kwa risasi, ambapo mmoja alikufa na mwingine alifanikiwa kukimbia.
Majambazi hao walimvamia Mwakyusa kwa lengo la kuiba mali nyumbani kwake. Hata hivyo, hawakufanikiwa kupora mali yoyote baada ya wawili hao kujeruhiwa, hivyo wengine kukimbia.

Kamanda Minangi alisema tayari watuhumiwa watatu, wameshakamatwa na upelelezi unaendelea ili kuwakamata wengine, waliohusika katika tukio hilo.

"Ni kweli tukio hilo limetokea na anadai walikuwa saba na mmoja alikuwa na bunduki, yeye pia alikuwa na silaha hivyo aliweza kujihami ambapo aliwajeruhi wawili mmoja kwa nje na mwingine aliyekuwa ameingia chumbani kwake," alisema Kamanda Minangi.

Alisema mmoja kati ya hao waliojeruhiwa, alikufa akiwa njiani kupelekwa  hospitalini, maiti amehifadhiwa katika Hospitali ya Amana.

Alisema majeruhi mwingine, alikamatwa asubuhi wakati amekwenda kuomba Fomu Maalumu ya Matibabu ya Polisi (PF3) katika kituo cha Polisi Gongo la Mboto.

"Alipofika kuomba PF3 alidanganya kuwa ameporwa pikipiki na majambazi  ambao walimjeruhi, lakini alitiliwa shaka na baada ya kuhojiwa zaidi alikiri kuhusika katika tukio hilo na akawekwa chini ya ulinzi, wengine wawili walikamatwa katika maeneo tofauti," aliongeza.

Kamanda Minangi alisema mahojiano yanafanyika kwa hao waliokamatwa, ili kubaini wengine waliohusika ili pia waweze kukamatwa na sheria kuchukua mkondo wake.

Alisema katika tukio hilo, Mwakyusa na familia yake hawakujeruhiwa wala kupata matatizo yoyote kutoka kwa majambazi hao.

Akizungumza kwa njia ya simu na mwandishi, Mwakyusa alisema, "Wakati wameshaingia ndani walikuwa wanajiita majina yenye vyeo sawa na vile vya jeshi au polisi. Walikuwa wanaitana komandoo, kamanda na mengine ambayo ni sawa na vyeo".

No comments:

Post a Comment