TAFUTA CHOCHOTE NDANI YA NKEMA

Wednesday, 20 November 2013

Interpol wamtia nguvuni mwenye ghala la vipusa vya ndovu, Polisi Zanzibar

Na Mohammed Mhina, Jeshi la Polisi

Makachero wa Polisi Zanzibar kwa kushirikiana na Makachero wa Interpol, wamemkamata mfanyabiashara wa mjini hapa kwa tuhuma za usafirishaji wa meno ya tembo yaliyokamatwa wiki iliyopita kwenye kontena.

Kamishna wa Polisi wa Zanzibar, Mussa Ali Mussa, alimtaja mfanyabiashara huyo kuwa ni Mohammed Haji Haji Udole (41), mkazi wa Mbuzini mjini hapa.

Alisema mtuhumiwa huyo anadaiwa kuwa ni mmoja kati ya watu walioshiriki katika kuyapokea, kuyahifadhi na kuyaandaa 
meno hayo kwa ajili ya kusafirishwa.

Kukamatwa kwa mfanyabiashara huyo kunaifanya idadi ya watuhumiwa waliokwisha kamatwa kufikia sita baada ya wengine watano wakiwamo watumishi wawili wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na mmoja wa Mamlaka ya Bandari Zanzibar, kumatwa siku ya pili ya tukio hilo.

Mtuhumiwa Udole, anamiliki ghala kubwa la kuhifadhia mizigo katika eneo la Mbuzini mjini hapa.

Tayari mtuhumiwa Udole naye ameshasafirishwa kwenda Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Dar es Salaam kuunganishwa na watuhumiwa wengine watano waliokamatwa.

Watuhumiwa wengine katika sakata hilo ambao wanaendelewa kuhojiwa na makachero wa Polisi Makao Makuu jijini Dar es Salaam ni Mohammed Suleiman Mussa (45) na Juma Ali Makame (34), ambao ni mawakala wa mizigo kutoka Kampuni ya Island Sea Food ya Zanzibar.

Wengine ni Omari Hamad Ali (50) na Mohammed Hija (48), ambao ni maofisa wa TRA tawi la Zanzibar na Haidar Ahmad Abdallah (54), mfanyakazi wa Bandari ya Zanzibar.

Meno hayo ambayo yalikamatwa Jumatano iliyopita Novemba kwenye Bandari ya Zanzibar, ni vipande 2,023 vyenye uzito wa kilo 2,915 yaliyotokana na kuuawa kwa tembo 305 wenye thamani ya Dola za Marekani 4,775,000 (sawa na Sh. bilioni 7.4).

Vipande hivyo vya meno vilikuwa kwenye magunia 98 yaliyochanganywa na viumbe vya Bahari na kuwekwa kwenye konteina la futi 40 yakiwa tayari kusafirishwa kwa meli ya MV Kota Henning kwenda Ufilipino. --- via blogu ya ZanziNews

No comments:

Post a Comment