JESHI la Polisi wilayani Bunda, jana lililazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wananchi wenye hasira kali waliotaka kumuua mwanamke mmoja mkazi wa mtaa wa Cha Nyerere katika mamalaka ya mji mdogo wa Bunda.
Mwenyekiti wa mtaa huo, Maxmilian Bwire, alisema kuwa tukio hilo lilitokea saa 10 usiku nyumbani kwa mwanamke huyo, Sarafina Nyamboko, maarufu kama mama Nyamboko.
Alisema kuwa siku ya tukio mama huyo alikutwa na mpangaji wake, Robert Msilimu, akiwa uchi wa mnyama na kopo tupu la amboni lita tano, lililodaiwa kuwa na dawa ambayo alikuwa ameimwaga katika kila mlango wa wapangaji wake.
“Baada ya kumhoji alisema alikuwa anawamwagia dawa ya baraka wapangaji wake kwani kila tarehe moja huwa anafanya hivyo ili waweze kupata baraka kwa Mwenyezi Mungu.
“Dawa hiyo inaonekana ilikuwa imechanganyikana na kinyesi maana mji mzima ulikuwa unanuka kinyesi,” alisema mpangaji huyo ambaye alimkuta mwenyenyumba wake akifanya mchezo huo.
Alifafanua kuwa kitendo hicho kilimshtua sana ndipo alipowaamsha wapangaji wenzake ambao waliamua kupiga yowe na majirani walifika na silaha mbalimbali za jadi na kuanza kumshambulia.
Alisema kwa kushirikiana na mwenyekiti wa mtaa huo, walipiga simu polisi ambao walikuja na baada ya kukuta hali ni mbaya, waliamua kutumia mabomu ya machozi ili kuwatawanya wananchi hao na kumchukua mama huyo kwenda naye kituo cha polisi.
Hata hivyo, baadhi ya majirani walidai kuwa hii ni mara ya tatu sasa kwa mama huyo kukutwa anafanya mchezo huo na kwamba hata kwenye mikutano ya hadhara ya mtaa huo, ameshaonywa mara kwa mara lakini alikuwa hajaacha.
Polisi walisema kuwa wanaendelea kumhoji kwa kina kuhusu kitendo hicho cha kukutwa uchi na pia kufahamu ukweli wa dawa hiyo aliyokutwa nayo.
Kama ikithibitika kuwa kuna kosa ndani yake watamfikisha kwenye mkondo wa sharia.
No comments:
Post a Comment