JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA AFYA NA USTAWI WA JAMII
TAMKO LA SERIKALI KUHUSU TETESI ZA KUWEPO MGONJWA ANAYEHISIWA KUWA NA UGONJWA WA EBOLA WILAYANI SENGEREMA MKOANI MWANZA
20 Oktoba 2014
Utangulizi
Mgonjwa huyu alilazwa katika Kituo cha Afya Mwangika tarehe 15 hadi 16 Oktoba, 2014 ambapo pia alionekana kuwa vimelea vya ugonjwa wa Malaria kabla ya kuhamishiwa Hospitali Teule ya Wilaya ya Sengerema mnamo tarehe 17 oktoba 2014 na kufariki duniani siku hiyo hiyo muda wa saa 3.30 usiku.
Hata hivyo, mgonjwa huyu hakuwa na historia ya kusafiri kwenda nchi zilizoathirika na ugonjwa wa Ebola na hakuwahi kupokea mgeni kutoka nchi hizo ndani ya siku ya 21 zilizopita.
Hatua zilizochukuliwa ni pamoja na;
i.Sampuli ya damu ya mgonjwa kwa ajili ya uchunguzi wa Kimaabara ilipokelewa tarehe 18 Oktoba, 2014. Matokeo ya awali dhidi ya magonjwa ya jamii ya ebola yakiwa ni pamoja na Dengue na Chikungunya yanaonyesha kuwa mgonjwa hakuwa na magonjwa haya. Uchunguzi wa kimaabara bado unaendelea na Wizara itatoa taarifa rasmi pindi utakapokamilika.
ii.Mgonjwa alihudumiwa katika chumba maalumu kilichotengwa ambapo wahudumu pamoja na walioshughulikia mazishi yake walivaa vifaa kinga (PPE)
iii.Wataalamu pamoja na ndugu waliomhudumia mgonjwa kabla ya mauti kumfika wametengwa na wapo kwenye uangalizi maalumu
Mwongozo wa utambuzi wa ugonjwa huu (Standard Case Definition) unaeleza kwamba ili mgonjwa aweze kuhusiwa kuwa na ugonjwa wa Ebola anatakiwa akidhi vigezo ifuatavyo:
i. Dalili za awali ni homa kali ya ghafla, kulegea mwili, maumivu ya misuli, kuumwa na kichwa, na kutokwa na vidonda kooni. Mara nyingi dalili hizi hufuatiwa na kutapika, kuharisha,kutokwa na vipele vya ngozi, kwa baadhi ya wagonjwa hutokwa na damu ndani na nje ya mwili
ii.Awe amesafiri kwenda sehemu zilizothibitishwa kuwa na ugonjwa wa ebola ndani ya kipindi cha wiki 3
iii. Kugusa majimaji kutoka kwa mgonjwa, maiti au mnyama anayehisiwa au kuthibitishwa kuwa na ugonjwa wa Ebola.
Hitimisho
Wizara inapenda kuwatoa hofu wananchi kuwa hadi sasa HAKUNA MGONJWA yeyote aliyethibitishwa kuwa na virusi vya ugonjwa wa Ebola hapa nchini. Hata hivyo uchunguzi wa kina wa Kimaabara unaendelea na taarifa itatolewa baada ya majibu kupatikana.
Wananchi wanashauriwa kutokuwa na hofu ila kuendelea kuchukua tahadhari za kuepuka kupata maambukizi ya ugonjwa huu ambazo:-
- Kuepuka kugusa au kuingiwa na mate, damu, mkojo, jasho, kinyesi, machozi na majimaji mengine yanayotoka mwilini mwa mwenye dalili za ugonjwa wa Ebola kupitia sehemu zenye michubuko au vidonda.
- Kuepuka kushughulikia maiti ya mtu aliyekufa akiwa na dalili za ugonjwa wa Ebola; badala yake watoe taarifa kwa uongozi wa kituo cha huduma za Afya kwa ushauri. Wataalam watasimamia maziko ikiwa itatokea.
- Wananchi waepuke mila na desturi zinazoweza kuchelewesha kupata huduma muhimu na kuzidi kueneza ugonjwa wa Ebola.
- Kutoa taarifa mapema kwa viongozi wa Serikali na watoa huduma za Afya katika ngazi zote pale anapotokea mtu mwenye dalili za ugonjwa wa Ebola.
- Kuwahi katika vituo vya kutolea huduma za Afya pale mtu anapohisiwa kuwa na dalili za ugonjwa huu.
Imetolewa na,
Dkt. Donan Mmbando
KAIMU KATIBU MKUU
20 Oktoba, 2014
Dkt. Donan Mmbando
KAIMU KATIBU MKUU
20 Oktoba, 2014
No comments:
Post a Comment