TAFUTA CHOCHOTE NDANI YA NKEMA

Thursday, 16 October 2014

KIZUNGUMKUTI KURA YA MAONI:AG KUPASUA JIPU.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji FrederickWerema

Msimamo rasmi wa serikali kuhusu kura ya maoni kuamua ama kuikubali au kuikataa katiba inayopendekezwa, iwapo itapigwa kabla au baada ya uchaguzi mkuu ujao, unatarajiwa kutangazwa leo.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema, aliliambia NIPASHE jana kuwa ataweka bayana msimamo wa serikali leo ili kuzima mkanganyiko uliojitokeza kuhusiana na lini kura hiyo itapigwa.

Mkanganyiko huo unafuatia Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), John Cheyo, kueleza kwamba walikubaliana na Rais Jakaya Kikwete katika kikao kati yake na viongozi wakuu wa vyama vya siasa kuwa mchakato wa upigaji kura hiyo uahirishwe ili kutoa nafasi ya kufanyika maandalizi ya uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu ujao.

Lakini Rais Kikwete jana alisema serikali ipo kwenye maandalizi ya kuandaa utaratibu wa kuipigia kura ya maoni ‘katiba’ hiyo. 

Jaji Werema alisema jana kuwa wananchi wanapaswa kuwa na subira hadi hapo msimamo rasmi wa serikali kuhusiana na suala hilo utakapotolewa leo. 

Alisema hayo alipotakiwa na NIPASHE kueleza msimamo unaoeleweka dhidi ya mkanganyiko uliojitokeza kuhusiana na suala hilo.

“Swali nzuri. Subiri hadi kesho. Ninao ufunguo wa subira…Subira yavuta heri! Aogeleaye ni mweye utulivu. Papara sumu ya maji,” alisema Jaji Werema akijibu swali la mwandishi jana.

CHEYOWakati Jaji Werema akisema hayo, Cheyo jana alisema TCD itaitisha mkutuno ili kujadili kauli iliyotolewa na Rais Kikwete kwamba, serikali inaanda mchakato wa kupigiwa kura ya maoni katiba inayopendekezwa.

 Cheyo, ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama cha UDP na Mbunge wa Bariadi Mashariki, alisema suala hilo ni la kujadili wote kwa kuwa kulikuwa na makubaliano ya kusitisha mchakato wa katiba mpya mpaka uchaguzi mkuu ujao.

NECTume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) imesema wiki ijayo itaitisha mkutano na waandishi wa habarikuzungumzia masuala mbalimbali, ikiwamo maandalizi ya kura ya maoni kwa katiba inayopendekezwa.

Mkurugunzi wa Uchaguzi wa Nec, Julius Mallaba, alisema mambo yote watayazungumzia wiki ijayo.“Hayo mambo ni mazito na mara kwa mara nimekuwa nikipigiwa simu kuuliziwa na waandishi mbalimbali. Wiki ijayo tutawaeleza ili muwajulishe wananchi,” alisema Mallaba.

CUFKaimu Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Joran Bashange, alisema hawakubaliani na kauli hiyo ya Rais Kikwete.

Alisema wakati wa makabidhiano ya katiba inayopendekezwa mjini Dodoma, Rais alisema, aliombwa kusogezwa mbele muda wa kupiga kura ya maoni, lakini sasa amegeuka.

Bashange alisema walikubaliana na Rais Kikwete katika kikao hicho kwamba, kura ya maoni ifanyike baada ya uchaguzi mkuu mwakani baada ya kufanyika kwa baadhi ya marekebisho kwenye daftari la kudumu la wapigakura.

“Akiwa Dodoma alisema tulikubaliana hadi mwakani baada ya uchaguzi mkuu, ndipo upigaji kura ya maoni ufanyike. Juzi alikubali, jana (juzi) amegeuka. Pana tatizo, kuna ombwe,” alisema Bashange.

Aliongeza: “Hata kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa, alisema ungefanyika kati ya Februari na Machi, mwakani baada kufanyika kwa marekebisho hayo. Tume yenyewe  ilisema hadi waboreshe dafatari hilo Mei, mwakani. Hatuko tayari, msingi daftari liwepo.”

KAULI YA JKJuzi wakati akihutubia wananchi kwenye sherehe za kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru na kumbukumbu ya miaka 15 ya kifo cha Baba wa Taifa, Hayati Julius Nyerere, katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, mjini Tabora, Rais Kikwete alisema mchakato wa kupatikana katiba mpya nchini umepita hatua kubwa na kwa sasa serikali ipo kwenye maandalizi ya kuandaa utaratibu wa kuipigia kura ya maoni. 

“Mchakato wa kupatikana katiba mpya umepitia hatua kubwa na sasa serikali ipo katika maandalizi ya utaratibu mzuri wa kupiga kura ya maoni kwa katiba inayopendekezwa,” alisema Rais Kikwete.

Aliongeza: “Hii ni zaidi ya Katiba nzuri, ni bora kuliko tuliyonayo sasa, tumeiboresha sana, tumeimarisha tunu, ina mambo mazuri tangu tulikotoka  hadi tulipo sasa. Imeweka misingi mizuri kulingana na wakati tulio nao na inatoa majibu ya changamoto tunazokabiliana nazo sasa. Ni Katiba ya wananchi wote…..ombi langu kwenu…jitokezeni kuipiga kura za ndiyo.

Aliwataka Watanzania, wakiwamo vijana kujitokeza kwa wingi wakati wa upigaji wa kura za maoni, kwani Tanzania imo mikononi mwao. KAULI YA PINDAKauli hiyo ya Rais Kikwete ya juzi ilitanguliwa na ile iliyotolewa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ambaye alisema atafurahi kuona mchakato mzima wa katiba ukikamilika kabla rais mpya hajapatikana katika uchaguzi mkuu ujao.

Pinda alitoa kauli hiyo katika Bunge Maalumu la Katiba baada ya kupewa nafasi na Mwenyekiti wa Bunge hilo kutoa shukrani na kupendekeza kura ya maoni ipigwe sambamba na Rais Kikwete ili kiongozi ajaye afanye kazi ya kutekeleza matakwa ya katiba hiyo.

Alisema rais ajaye anaweza kuwa na ajenda zake, hivyo ni muhimu kumaliza kazi yote na kumkabidhi katiba, ambayo imekamilika ili aitekeleze.
“Nampongeza sana mwenyekiti kwa kufanya kazi nzuri ya kuhakikisha katiba inayopendekezwa inapatikana kwa wakati na kwa kuzingatia maoni ya wananchi,” alisema Pinda.

KAULI YA AWALI YA CHEYOKabla ya hapo, Septemba 9, mwaka huu, Cheyo akizungumza na waandishi wa habari akiwa amefuatana na Mwenyekiti wa TLP, Augustino Mrema, Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Philip Mangula na Mwenyekiti wa UPDP, Fahami Dovutwa, alisema kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba mwisho wa mchakato wa upatikanaji wa katiba mpya ni kura ya maoni.

Cheyo, alisema katika mkutano na waandishi wa habari alisema kura hiyo ingefanyika Aprili, mwakani, lakini kikao hicho na Rais Kikwete kimeona endapo mchakato huo utaendelea hadi kura ya maoni, ungeathiri uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika nchini Oktoba, mwakani.

“Kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, baada ya Bunge Maalum kumaliza kutunga katiba ingefuata hatua ya kura ya maoni kuthibitisha katiba, kwa kutambua kuwa hatua ya kura ya maoni italazimisha uchaguzi mkuu 2015 kuahirishwa, tumekubaliana hatua hii iahirishwe,” alisema Cheyo.

Aliongeza: “Kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, mwisho wa mchakato ni kura ya maoni itakayofanyika Aprili 15 na kama itabidi kura irudiwe kwa mujibu wa sheria iliyotajwa, kura itarudiwa Juni au Julai, 2015 muda ambao Bunge la Jamhuri la Muungano linatakiwa livunjwe kwa ajili ya uchaguzi mkuu.”

Alisema ili katiba mpya itumike katika uchaguzi mkuu unaokuja itabidi uhai wa Bunge na Serikali uongezwe zaidi ya mwaka 2015 jambo, ambalo hawaliungi mkono.

Cheyo, alisema baada ya kupatikana katiba inayopendekezwa hatua inayofuata, ambayo ni kura ya maoni ambayo ilikuwa ifanyike Aprili, mwakani itasitishwa na kusogezwa mbele na kuendelea tena baada ya uchaguzi mkuu Oktoba, mwakani.

SHERIA INASEMAJE?
Hata hivyo, wakati kukiwapo wasiwasi kuhusiana na lini kura ya maoni itafanyika, Sheria ya Kura ya maoni ya mwaka 2013, inaelekeza kwamba kura ya maoni ifanyike siku 84 tangu kukabidhiwa kwa Katiba inayopendekezwa kwa Rais.
Chanzo;Nipashe

No comments:

Post a Comment