TAFUTA CHOCHOTE NDANI YA NKEMA

Thursday, 19 December 2013

MBEYA:Mamlaka ya udhibiti wa chakula,dawa na vipodozi(TFDA) kanda ya nyanda za juu kusini imezifunga machinjio mbili Mkoani humo.



Hii ni machinjio ya Mbalizi iliyofungwa



Kaimu Meneja wa Kanda nyanda za juu Kusini,Rodney Alananga, alithibitisha kufungiwa kwa machinjio hizo na kwamba sababu za kufunga machinjio ya Uyole Jijini Mbeya ni kutokana na  kutokuwa na miundo mbinu mizuri ya maji hivyo kuhatarisha afya za walaji na wakazi walio kando ya machinjio.

 Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Magreth Akilimali, alilazimika kutembelea na kujionea hali halisi ya uchafu uliokithiri na kuahidi kuwa watafanya usafi eneo hilo kwa muda wa siku tano kuanzia Desemba 14 kwa kutumia gari la kunyonya maji machafu la Halmashauri ya Jiji la Mbeya.







MAMLAKA ya udhibiti wa chakula,dawa na vipodozi(TFDA) kanda ya nyanda za juu kusini imezifunga machinjio mbili Mkoani Mbeya kutokana na kuwa na kasoro za kiafya.


Machinjio hizo ni Uyole iliyopo Jijini Mbeya na Mbalizi iliyopo katika Wilaya ya Mbeya Mkoani hapa kutoka na kukithiri kwa uchafu.


Kaimu Meneja wa Kanda nyanda za juu Kusini,Rodney Alananga, alithibitisha kufungiwa kwa machinjio hizo na kwamba sababu za kufunga machinjio ya Uyole Jijini Mbeya ni kutokana na  kutokuwa na miundo mbinu mizuri ya maji hivyo kuhatarisha afya za walaji na wakazi walio kando ya machinjio.


Alananga amebainisha kuwa machinjio hiyo haina uzio na kufanya watu wasiohusika kuingia machinjioni kinyume na sheria kwani watu wanaopaswa kuingia ndani ya machinjio ni wahusika tu.


Alisema  kabla ya kufunga machinjio hayo ya Uyole mara kadhaa waliongea na uongozi wa Jiji la Mbeya lakini hawakutekeleza maagizo waliyopewa mara kwa mara na hivyo Mamlaka kuamua kuifunga ili kuokoa afya za wananchi wasikumbwe na magonjwa kama kuhara na kipindupindu.


Alisema sababu nyingine ni kujaa kwa mashimo ya maji machafu kutokana na kutokunyonywa kwa muda mrefu hali inayosababisha harufu mbaya eneo hilo na maeneo yanayozunguka na kuleta uchafuzi wa mazingira Jijini.


Kwa upande wa Machinjio ya Mbalizi, Alananga alisema sababu za kufunga  ni pamoja na wafanyakazi wa Halmashauri kutokuwa na sare za kufanyia kazi kama viatu vyeupe,kofia na makoti meupe kama sheria inavyoagiza.


Alisema kuwa hali ni mbaya zaidi katika machinjio hiyo kutokana na mashimo kujaa kwa muda mrefu hivyo maji machafu na taka kufurika na kutiririsha uchafu mto Mbalizi na kuwafanya wananchi wanaotumia maji ya mto huo kuwa hatarini kukumbwa na magonjwa kutokana na  wengine huyatumia kunywa kutokana na uhaba wa maji ya bomba bonde la Mbalizi.


Kutokana na  hali hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Magreth Akilimali, alilazimika kutembelea na kujionea hali halisi ya uchafu uliokithiri na kuahidi kuwa watafanya usafi eneo hilo kwa muda wa siku tano kuanzia Desemba 14 kwa kutumia gari la kunyonya maji machafu la Halmashauri ya Jiji la Mbeya.


Hata hivyo Akilimali,  alipoulizwa  sababu za kufungwa Machinjio hakuwa tayari kuongea eneo la tukio na kudai kuwa afuatwe ofisini kwake ambapo aliamua kuingia katika gari lake na kuondoka eneo la tukio.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa machinjio ya Mbalizi, Simon Petro(Mwadada) alisema amesikitishwa na kitendo cha kufungwa kwani kitendo hicho kimewatia hasara kubwa kwa madai kuwa itawalazimu kutumia zaidi ya shilingi elfu sitini kwenda kuchinja machinjio ya Mjini au Songwe.

Baadhi ya wafanya biashara ya nyama eneo la Mbalizi akiwemo Sikujua Mwambambe ameishukia Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya kwa kutofanya usafi licha ya Madaktari wa mifugo kupima nyama kila siku na kukusanya ushuru hali inayoonesha kuna hali ya uzembe na uwajibikaji hafifu kutokana na  taarifa zimepelekwa ofisini lakini hakuna utekelezaji wowote.


Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mbeya, Anderson Kabenga, amekiri kufungwa kwa machinjio hiyo na kwamba amemwagiza Mkurugenzi kufanya zoezi la usafi haraka ili kuondoa usumbufu kwa wakazi wa Mbalizi na kitendo hicho kinaipunguzia mapato Halmashauri.


Kabenga alisema wanatafuta machinjio mbadala ili huduma za uchinjaji ziendelee katika kipindi hiki cha ukarabati.


Kwa upande wake Kaimu Meneja wa TFDA kanda ya nyanda za juu Kusini, Alananga alisema  zoezi hilo ni kutekeleza sheria ya chakula,Dawa na vipodozi sheria namba 41,43 na 44 ya mwaka 2003 na kwamba Mamlaka itaendelea kufanya ukaguzi katika maeneo mengine.


Mamlaka hiyo kwa siku za hivi karibuni imeteketeza vyakula,dawa na vipodozi hatari vilivyokwisha muda wake na vilivyoingizwa nchini kinyume cha sheria katika wilaya za Momba,Kyela na Jijini Mbeya.

Na Mbeya yetu

No comments:

Post a Comment