Profesa, Sospeter Muhongo |
WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amesema mwenye mamlaka ya kutoa mikataba ya wawekezaji kuhusu Wizara hiyo na wawekezaji ni yeye, hivyo Kamati ya Kuduma ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), chini ya Zitto Kabwe haikufuata utaratibu ilipoagiza Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Michael Mwanda na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, James Andilile kuwapatia mikataba hiyo.
Profesa Muhongo alitoa kauli hiyo leo wakati akijibu maswali ya waandishi kuhusu TPDC kugoma kuipatia PAC mikataba wakati huo huo akijinadi kuwataka wawekezaji kuzingatia uwazi katika mikataba wanayoingia na Serikaki.
Alisema alipopewa taarifa na TPDC alishauriana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) ambapo walikubaliana kutotoa mikataba hiyo kwa kile alichodai kuwa utaratibu uliotumika haukuwa sahihi na mikataba ni siri kati ya mwekezaji na Serikali.
Muhongo alisema haipo sababu ya kukataa kutoa mikataba iwapo utaratibu utafuatwa lakini si jambo la kila mtu akitaka kupewa atapewa kwani sio utaratibu wa kutoa mikataba ulivyo duniani kote.
"Nakiri kuwa TPDC wa iliniletea barua ya kuomba mikataba ya gesi na mafuta ila baada ya kuwasiliana na Mwanasheria tuliona hakuna utaratibu uliofuatwa katika mchakato huo," alisema.
Alisisitiza kuwa utaratibu uko wazi kuwa Waziri ndiye mamlaka ya kutoa mikataba hiyo ila ni baada ya kukubaliana na wahusika kwani kutofanya hivyo kunaweza kusababisha kushitakiwa.
"Jamani suala la mikataba ni baina ya kampuni na Serikali hivyo kwenda kinyume na tafsiri hiyo ni wazi kuwa tunahitaji Serikali kushtakiwa na wawekezaji," alisisitiza Waziri.
Alisema ni vema Watanzania wakajiepusha na ushabiki katika masuala ya kitaalamu kwani unaweza kufikisha nchi pabaya.
Profesa Muhongo alisema wapo Wabunge ambao wamekuwa wakishabikia na kusema nchi za nje zinaweka mikataba wazi jambo ambalo halina ukweli.
"Mimi nimeishi nje miaka mingi watuambie ni nchi gani ambayo inatoa mikataba ambayo imesainiana na wawekezaji waambie waache kudanganya wananchi," alisema. (Imeandaliwa na mtandao wa www.habari za jamii.com-simu namba 0712-727062)
No comments:
Post a Comment