Baadhi ya washiriki wa Semina ya Usambazaji wa Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012 wakifuatilia masuala mbalimbali leo mkoani Pwani.
Kamishna wa Sensa ya Watu na Makazi 2012 Hajjat Amina Said Mrisho akimkabidhi machapisho ya Sensa Mkuu wa Mkoa wa Pwani Bi. Mwantumu Mahiza (aliyekaa) akizindua rasmi Usambazaji wa Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012 leo mkoani Pwani.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Bi. Mwantumu Mahiza (aliyekaa) akizindua rasmi Usambazaji wa Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012 leo mkoani Pwani. Nyuma yake ni viongozi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu wakiongozwa na Mkurugenzi Mkuu Dkt. Albina Chuwa (kushoto).
Baadhi ya washiriki wa Semina ya Usambazaji wa Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012 wakiangalia moja ya ramani inayoonyesha takwimu ya Mgawanyo wa Watu kwa umri na Jinsi na taarifa za Msingi za Kidemografia, Kijamii na Kiuchumi.
Washiriki wa Semina ya Usambazaji wa Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012 wakiangalia moja ya ramani inayoonyesha takwimu ya Mgawanyo wa Watu kwa umri na Jinsi na taarifa za Msingi za Kidemografia, Kijamii na Kiuchumi.
Washiriki wa Semina ya Usambazaji wa Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012 wakiwa katika picha ya pamoja.
Picha na Habari na
Aron Msigwa–MAELEZO
Ofisi ya Taifa ya Takwimu imezindua rasmi usambazaji wa matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 na kuwataka wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa wilaya na mikoa kote nchini kuanza kutumia na kuhamasisha matumizi ya takwimu rasmi zilizotolewa na ofisi hiyo katika kupanga mipango ya maendeleo.
Hayo yamebainishwa leo mkoani Pwani na Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa wakati akiwakaribisha viongozi, watendaji na wadau mbalimbali wa mkoa wa Pwani waliohudhuria semina ya usambazaji wa Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012.
Amesema Tanzania ina takwimu bora kutokana na kazi kubwa iliyofanywa na Ofisi yake kwa kushirikiana na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuandaa na kukamilisha taarifa za matokeo ya Sensa yakiwemo machapisho matatu yanayohusu Idadi ya Watu katika ngazi ya Utawala, chapisho la Mgawanyo wa Watu kwa umri na Jinsi na chapisho la Taarifa za Msingi za Kidemografia, Kijamii na Kiuchumi.
Dkt. Chuwa ameeleza kuwa Ofisi ya Taifa ya Takwimu inaendelea na mikakati mbalimbali ya kuhamasisha matumizi ya takwimu za matokeo ya Sensa katika ngazi ya mkoa, wilaya na vijiji ili ziweze kutumika katika kupanga mipango ya maendeleo.
Ameeleza kuwa takwimu zitakazowasilishwa katika maeneo mbalimbali katinga ngazi ya kijiji, wilaya na mikoa ukiwemo mkoa wa Pwani ambao umezindua rasmi shughuli hiyo ya usambazaji wa matokeo zitahusu Umri, Jinsi na Viashiria muhimu vya umri katika makundi, hali ya ndoa, hali ya uyatima na vifaa vilivyotumika katika ujenzi wa nyumba .
Amesema lengo la usambazaji wa takwimu hizo ni kueleza hali halisi ya mafanikio ya mikoa katika Nyanja za uchumi, umasikini, elimu na afya ili kuwezesha uboreshaji wa maeneo ambayo hayafanyi vizuri.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani Bi. Mwantumu Mahiza akizindua rasmi Usambazaji wa Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012 kwa ngazi ya vijiji, Wilaya na mikoa ameeleza kuwa usambazaji wa matokeo hayo utawasaidia na kuwarahisishia viongozi wa maeneo mbalimbali kupanga Bajeti na mipango ya maendeleo.
Amesema matumizi ya takwimu sahihi yatawezesha upelekaji wa huduma za jamii zikiwemo shule, hospitali, ujenzi wa masoko, huduma za maji na kuirahisishia serikali kuwafikishia wananchi huduma hizo kutokana na takwimu zilizoainishwa katika maeneo husika na kuiepusha serikali kuwekeza fedha nyingi katika miradi ambayo haiendani na idadi ya watu katika eneo husika.
Ameongeza kuwa matumizi ya takwimu hizo kuanzia ngazi ya familia hadi taifa yatasaidia kupunguza na kuondoa migogoro ya ardhi hususani kurahisisha suala la umiliki na mgawanyo wa ardhi kulingana na idadi ya watu na huduma.
Bi.Mahiza ametoa wito kwa viongozi mbalimbali wa serikali na madhehebu ya dini kote nchini kuwahamasisha wananchi kutumia takwimu zitakazosambazwa katika maeneo mbalimbali nchini.
Naye mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu Duniani (UNFPA) nchini Tanzania Bw.Colins Opiyo akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina hiyo amesema kuwa UNFPA itaendelea kushirikiana na Tanzania ili kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa na takwimu sahihi.
No comments:
Post a Comment