TAFUTA CHOCHOTE NDANI YA NKEMA

Sunday 1 December 2013

UDSM-DUCE wamsimamisha uongozi Dk Kitila Mkumbo (?)

Taarifa zinasema kuwa uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam umemvua kwa muda Mhadhiwa Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Kitila Mkumbo madaraka ya kuongoza Kitivo cha Elimu cha Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu cha Dar es Salaam (DUCE).

Hatua hiyo inatajwa kuchukuliwa baada ya uongozi wa UDSM kupata taarifa kwenye vyombo vya habari kuwa Dk Kitila Mkumbo alikuwa kiongozi wa chama cha siasa, CHADEMA wakati angali ni mtumishi wa umma, jambo ambalo Uongozi wa chuo hicho umekariri kuwa ni kinyume cha sheria ya nchi na Serikali kwa mfanyakazi wa umma kushika wadhifa katika chama cha siasa.

Kutokana na uamuzi wa chuo hicho, Dk Kitila aliandikiwa na kukabidhiwa barua ya kusimamishwa kwake wadhifa huo.

Dk Kitila bado ataendelea kuwa Mhadhiri Mwandamizi kwenye kitivo hicho.

Hii imenikumbusha habari ya Asha Bani iliyochapishwa kwenye gazeti la Tanzania Daima tarehe 14 Januari 2010 ikisema:



"Prof. BAREGU APONZWA NA SIASA"

HATIMAYE serikali imesema imesitisha ajira ya aliyekuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Saalam, Profesa Mwesiga Baregu kutokana na kukiuka sheria ya utumishi wa umma.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Dar es Salaam jana, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Hawa Ghasia, alisema Profesa Baregu alikiuka maelekezo ya waraka mkuu namba moja wa Utumishi wa Umma wa mwaka 2000 ambao unakataza kujihusisha na masuala ya siasa.

“Waraka Mkuu wa Utumishi wa Umma namba moja wa mwaka 2000 unatoa maelekezo kuhusu maadili ya watumishi wa umma katika mfumo wa vyama vingi na ushiriki wa watumishi wa umma katika siasa ikiwemo miiko yake. Waraka huo pia 
unabainisha mambo yanayoruhusiwa na yale yasiyoruhusiwa kwa watumishi wa umma katika kushiriki siasa.

“Baadhi ya mambo yasiyoruhusiwa kwa watumishi wa umma ni kugombea nafasi yoyote chini ya katiba au uongozi wa ngazi yoyote katika chama cha siasa akiwa mtumishi wa umma,” alisema Ghasia.

Alisema Profesa Baregu akiwa kama mtumishi wa umma amekiuka waraka huo kwa kujihusisha na siasa kutokana na kuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya Taifa ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Ghasia alisema Baregu amekuwa akishikilia nafasi hiyo kwanza kama mjumbe wa kuteuliwa na mwenyekiti wa CHADEMA na sasa kama mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho baada ya kuchaguliwa na Baraza Kuu la CHADEMA mwezi Septemba mwaka jana.

“Kwa hiyo Profesa Baregu ni kiongozi wa CHADEMA na hivyo kukosa sifa ya kuendelea na utumishi wa umma. Utaratibu huu ni kwa watumishi wote wanaoamua kugombea nyadhifa mbalimbali za uongozi katika vyama vyote vya siasa,” alisema Waziri Ghasia.

Alisema haki ya Profesa Baregu ya kuajiriwa kama ilivyo kwa watumishi wote wa umma, ilikwisha pale alipostaafu kwa lazima na kwa mujibu wa sheria mwaka 1999.

“Akiwa kiongozi wa kisiasa, ajira yake kama mtumishi wa umma ilikuwa sharti ikome kwa mujibu wa kanuni na taratibu za ushiriki wa watumishi wa umma katika siasa,” alisema Ghasia.

Alisema utaratibu wa serikali unaruhusu baada ya mtumishi kustaafu kwa mujibu wa sheria mwajiri wake kulingana na mahitaji na inapothibitika kuwa hawezi kumpata mtumishi mwenye sifa kama hizo katika soko hulazimika kumwombea mstaafu ajira ya mkataba kwenye mamlaka husika.

Ghasia alisema kwa mujibu wa kanuni za utumishi wa umma mkataba wa ajira kwa mtumishi wa umma baada ya kustaafu kwa umri na kwa mujibu wa sheria, siyo haki ya mtumishi bali ni utashi na busara (discretion) ya mamlaka.

“Kwa kutumia utaratibu huu, Profesa Baregu alistaafu kazi kwa mujibu wa sheria tangu mwaka 1999 Februari 24 akiwa na umri wa miaka 55. Baada ya kustaafu ameajiriwa kwa mkataba na Chuo Kikuu Dar es Salaam mara tatu, aliajiriwa kwa mkataba wa mwaka mmoja Machi 21 mwaka 2003 baada ya kurejea kutoka Harare, Zimbabwe alikokuwa akifanya kazi tangu alipostaafu kazi,” alieleza Ghasia.

Aliendelea kueleza kama haitoshi alipewa mkataba mwingine wa kipindi cha miaka miwili ambacho kiliisha mwaka 2006 na kuongezewa mkataba mwingine ambao pia ulimalizika Januari 2008.

Waziri Ghasia ambaye hakutaka kuulizwa maswali zaidi ya matatu, akijibu swali kutoka kwa mwandishi wa habari aliyetaka kujua kama kuondoka kwa profesa huyo hakutakuwa na pengo katika taaluma na kwamba hakuna mhadhiri aliyeziba nafasi hiyo kwa sasa, alisema hadhani kama chuo hicho kinachojulikana duniani kote kitaanguka ama kushuka kwa kuondoka kwa profesa huyo.

“Kama Baregu ni bidhaa bora inayogombaniwa kwa nini iwe ni UDSM tu na asiende kwingine? Kwani ni lazima awe mhadhiri wa chuo hicho tu,” alihoji Ghasia.

Alipoulizwa kwanini serikali ilimuongezea Baregu mkataba mwaka 2006 huku ikijua fika anajihusisha na masuala ya siasa alisema: “Kosa lililofanyika wakati huo haliwezi kamwe kurudiwa kwa sasa.”

Alisema waraka huo haumbani mwanachama wa CHADEMA pekee bali wa vyama vyote vya siasa huku akitolea mfano kuwa hata Sara Msafiri alivyogombea ujumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi, aliondolewa katika utumishi wa umma.

Aliwataja makada wengine wa CCM waliobanwa na waraka huo kuwa ni Masauni Yusufu Masauni, aliyelazimika kuacha ajira yake katika Wizara ya Nishati na Madini na kugombea nafasi ya uenyeviti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM).

Alipoulizwa sababu za Waziri Mkuu kuendelea kuchukua pensheni (mafao) mara baada ya kustaafu, alijibu kuwa kama mtumishi wa umma waziri ana haki ya kuchukua pensheni kwa mujibu wa sheria.

“Mwandishi nimesema kuwa leo sitaki kujibu swali lingine zaidi ya kuzungumzia ajira ya Baregu, wewe unataka nikujibu hilo, nakwambia kama Waziri Mkuu ana haki ya kuchukua pensheni kama mtumishi wa umma pia, na usiulize swali jingine… kama umeshawapa na wenzako maswali wakashindwa kukuulizia vizuri utajua mwenyewe,” alijibu Ghasia kwa ukali.

Aidha mwandishi mwingine alipohoji sababu za Dk. Sengodo Mvungi kubakia kwenye ajira wakati anajihusisha kwenye masuala ya siasa, alijibu kuwa hata yeye naye hajaongezewa mkataba wake.

Akizungumzia suala hilo kwa njia ya simu, Profesa Baregu alishangaa kuchelewa kwa serikali kutolea ufafanuzi juu ya suala hilo kwani amekaa miezi sita bila kujua sababu za yeye kunyimwa mkataba tena.

Profesa Baregu alisema waraka huo una utata kutokana na kuwagusa wahadhiri ambao wako katika vyama vya upinzani na kuwaacha wengine waliomo CCM (majina yanahifadhiwa) wanaoendelea kufundisha chuoni hapo. “

Nitatafuta wanasheria ili wauchambue waraka huo kwa kina kwani unaonekana kutumika kibaguzi na kukwaza haki za msingi za raia,” alisema Profesa Baregu.

No comments:

Post a Comment