TAFUTA CHOCHOTE NDANI YA NKEMA

Thursday 17 October 2013

ROCK CITY MARATHON 2013, ZAIDI YA WANARIADHA 2000 KUSHIRIKI


 

ZAIDI ya wanariadha 2000 wanatarajia kushiriki mbio za mwaka huu, za awamu ya tano za Rock City, zitakazofanyika katika uwanja wa CCM Kirumba mkoani Mwanza mwezi Oktoba tarehe 27, kamati ya maandilizi imesema.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkuu wa kamati ya maandilizi ya mbio za Rock City mwaka huu, Bw. Mathew Kasonta alisema mwenendo wa usajili unaonyesha matumaini makubwa na kuongeza kuwa inatarajiwa kushika kasi zaidi katika wiki hii ya mwisho ambapo washiriki wanategemewa kuongezeka kufikia 2000 kwa mwaka huu.  

“Tunayo faraja kubwa kuona usajili unaendelea vizuri. Watu wengi wameshajitokeza kujisajili na kuchukua fomu wenyewe, na wengine wameshalipia fomu zao kupitia Airtel Money. Japokuwa usajili unaendelea, kwa mpaka jana, takwimu niliyo nayo inaonyesha kuwa wale waliochukua fomu zao wamefikia washiriki 531, wakati wengi waliotumia Airtel Money kulipia watachukua fomu zao wakati wowote kupitia vituo vifuatavyo; 

Makao Makuu ya Airtel jijini Dar es Salaam, Maduka ya Airtel Dodoma, Arusha, Mwanza, Zanzibar na Mbeya,” alisema. Mratibu wa mbio hizo alisema usajili bado unaendelea na fomu zinapatikana katika ofisi za kampuni ya Capital Plus International jijini Dar es Salaam, viwanja vya Nyamagana mkoani Mwanza na ofisi zote za michezo za wilaya mkoani Mwanza.

Kasonta alibainisha kuwa wanariadha kutoka nje wameonyesha nia yao ya kushiriki kwa kutuma maombi yao kupitia Chama cha Riadha Tanzania (RT) – ambacho kitahakikisha washiriki wote wa kutoka nje wanafuata taratibu zote za kisheria kabla ya kushiriki.

“Tumeshapata simu kutoka kwa washiriki kutoka nchi kama Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC), pamoja na washiriki ambao ni raia wa Australia, India, Canada na Amerika, wanaotaka kushiriki mbio hizi. Sababu tunafanyakazi kwa ukaribu na RT, tumeamua kuwa RT watahakikisha washiriki kutoka nje wanafuata taratibu zote kabla ya kushiriki ili kuifanya Rock City Marathon ifikie viwango vilivyowekwa kimataifa,” alisema Kasonta. Mbali na washiriki ambao tayari wamechukua fomu zao, Kasonta alisema makampuni mbali mbali, wafanyabiara, taasisi na watu maarufu wamethibitisha kuleta timu zao ili kushiriki mbio za kilometa 5 ambazo ni maalum kwa wafanyakazi.

Mratibu alisema kupitia udhamini wa NSSF, Africa Barrick Gold (ABG), Precision Air, Airtel kupitia Airtel Money, Bank M, PPF, Nyanza Bottling Ltd, New Mwanza Hotel, Sahara Communications, Continental Decoders na Umoja Switch, kamati imeboresha zawadi zitakazoshindaniwa na kualika kikundi cha Sanaa cha Bujora kitakachokuwepo kunogesha tukio hilo.

“Rock City Marathon ambayo kwa miaka mitano sasa imekuwa ikiandaliwa na kampuni ya Capital Plus International Ltd, kwa miaka mingi imekuwa ikibeba kauli mbiu ya “Tukuze utalii wa ndani kupitia michezo.” Kwa kutambua hilo, katika mbio za mwaka huu, tutaburudishwa na kikundi cha Sanaa cha Bujora ambacho kimeonyesha kuwa kikundi bora zaidi kwa kuonyesha utamaduni wa kitanzania kupitia dansi,” alisema.

Mbio za mwaka huu zinavipengele vitano ambavyo ni kilometa 21 kwa wanaume na wanawake, kilometa 5 kwa wafanyakazi kutoka katika makampuni, kilometa 3 kwa watu wenye ulemavu wa ngozi, kilometa 3 kwa wazee kuanzia miaka 55 na zaidi na kilometa 2 kwa watoto kuanzia umri wa 7 mpaka 10.

No comments:

Post a Comment