TAFUTA CHOCHOTE NDANI YA NKEMA

Monday 21 October 2013

PWANI :Visima nane kumaliza tatizo la maji,

 

Ofisa Uhusiano wa Dawasa, Nelly Msuya
*****
Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka jijini Dar es Salaam (Dawasa), inatekeleza mradi wa kuchimba visima virefu nane vya utafiti wa maji kwa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani, vitakavyogharimu Dola za Marekani Milioni 7.5, kwa lengo la kumaliza tatizo la maji kwa mikoa hiyo.

Akizungumza juzi, wakati wa ziara ya waandishi wa habari ya kukagua uchimbaji huo katika eneo la Kisarawe II Wilayani Temeke, Mkandarasi mwakilishi kutoka kampuni ya uchimbaji ya Zetas Zemin Teknolojisi, Dk. Mohamed Hassan, alisema visima hivyo vyote vitakamilika Mei mwakani.

“Hiki ni kisima cha kwanza na kinategemewa kutoa maji lita zipatazo milioni nane kwa siku. Kisima hiki pamoja na vingine, kitakuwa na kina cha urefu wa mita 600,” alisema na kuongeza kuwa uchimbaji wa visima hivyo utasaidia kujua uwezo wa visima vya maji jitakavyochimbwa maeneo ya Kimbiji badaye mwaka huu.


Alisema kisima kimoja kinachimbwa eneo la Mwasonga kilometa 36 kutoka jijini Dar es Salaam kimefikia urefu wa mita 530 ambacho kinakadiriwa kumalizika mwishoni mwa mwezi huu.

“Kiasi cha maji yatakayopatikana katika kisima hiki bado hakijafahamika ila mara baada ya kumalizika kazi hii ya uchimbaji tutafahamu uwezo wa maji uliopo, lakini tunakadiria kuwa siyo chini ya lita milioni nane kwa siku,” alisema Hassan.

Kwa upande wake Kaimu Msimamizi wa Ufundi wa Dawasa, John Kirecha, alisema mradi huo unatekelezwa katika maeneo ya Mwasonga, Kibada, Amanigoma, Mwanagati, Mgeule, Mzasa Chanika, Mkuranga na Amadori.

Alisema mradi mwingine wa uchimbaji wa visima 30 unategemea kuanza muda wowote kuanzia sasa baada ya kupata mkandarasi kutoka Iran.

Alibainisha kuwa visima 20 vitachimbwa Kisarawe II wakati visima 10 vitachimbwa Mpera na hivyo kumaliza tatizo la maji kwa mkoa wa Dar es Salaam na Pwani hadi mwaka 2032.

Ofisa Uhusiano wa Dawasa, Nelly Msuya, alisema mamlaka hiyo inatekeleza mpango wake wa kuhakikisha wananchi wa mikoa hiyo wanapata maji safi na salama.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment